Carousel

Breaking News

UMUHIMU WA FOLIC ACID





Folic acid ni aina ya Vitamini B9 ambayo huchanganyika na maji. Vitamini hii ni muhimu katika utengenezaji wa dutu za jeni (nucleic acid).

Vitamini hii ni mojawapo ya vitamini B complex, kama ilivyo vitamini B12. Vitamin B9 ni muhimu katika utengenezwaji wa seli hai nyekundu za damu, huzuia magonjwa ya uziwi(kupoteza kusikia), na hulinda afya ya ubongo mtoto aliye tumboni( mfumo wa fahamu wa mtoto).


Kwa nini folic acid ni muhimu?
Folic acid ni muhimu sana kwa wanawake walio wajawazito. Vitamin B9 inajumuisha dutu mbili nazo ni folate na folic acid ambazo ni muhimu kwa afya ya miili yetu.

Folic acid ni muhimu katika utengenezwaji wa seli hai nyekundu za damu pamoja na:
  • Utengenezwaji na ukarabati DNA na RNA ambazo ni dutu muhimu za jeni.
  • Husaidia mgawanyiko wa haraka wa seli hai katika mchakato wa ukuaji.
  • Husaidia kuimarisha afya ya ubongo, hususan kwa ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
  • Husaidia kutuepusha na matatizo ya kusikia yatokanayo na umri mkubwa.
Ni muhimu sana kwa wanawake walio wajawazito kutumia folic acid. Hii husaidia kuviepusha vijusi vilivyo tumboni dhidi ya ulemavu wa kuzaliwa kama wa ubongo au uti wa mgongo pamoja na kuwaepusha watoto na tatizo la mgongo wazi na kutokufunga kwa mfupa wa fuvu la kichwa (anencephaly).

Wanawake wanaotegemea ujauzito ni vyema kutumia folic acid au kula vyakula vyenye vitamini hii kwa wingi mwaka mzima kabla ya kupata ujauzito ili kupunguza hatari ya mtoto kupata magonjwa tuliyoyaona hapo awali. 
Folic acid husaidia kuimarisha mifupa na ubongo wa mtoto. Kwa hiyo wanawake wote walio wajawazito na wanaotegemea kupata ujauzito hawana budi kutumia folic acid.
Inashauriwa kila mwanamke ategemeaye kupata ujauzito atumie folic acid. Wanawake wenye miaka zaidi ya 14 wanahitajika kupata virutumisho vya folic acid kwa dozi ya microgramu 400 (mcg) kwa siku, na kiwango kiongezeke hadi microgramu 600 (mcg) wakati wa ujauzito. Na waendelee na microgramu 500 (mcg) kila siku wakati wa kunyonyesha.


Vyakula vyenye folic acid kwa wingi.
Vyakula vyenye folic acid kwa wingi ni kama kiini cha yai, mboga za kijani za majani na ni vyema kuepuka kupika katika joto kali na usitumie mafuta kwa kua hupunguza vitamini hii.

Vyakula vifuatavyo vinajulikana kuwa na kiwango kikubwa cha folic acid:
  • Hamira ya uokaji.
  • Brokoli
  • Kabichi
  • Parachichi
  • Ndizi mbivu
  • Kolimaua
  • Kiini cha yai
  • Figo
  • Dengu
  • Mboga aina ya chinese
  • Maini
  • Maziwa
  • Machungwa
  • Njegere
  • Alizeti
   Mkate wa ngano isiyokobolewa

Athari za upungufu
Mtu huwa na upungufu endapo kiwango cha folate na folic acid ni cha chini. Mbali na ugonjwa wa upungufu wa damu(anemia) mtu aupatao kutokana na upungufu wa folic acid pamoja na ulemavu wa kuzaliwa kwa watoto(congenital deformities) , pia yafuatayo ni magonjwa yasababishwayo na upungufu wa vitamini hii:

  • Mtu huwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa msongo.
  • Upotevu wa kumbukumbu na ufanyaji kazi wa ubongo.
  • Hatari ya kupata magonjwa ya mzio.
  • Udhaifu wa mifupa.


No comments